Joy FM

NGOs zatakiwa kuhudumia wananchi vijijini

11 February 2025, 10:38

Baadhi ya wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Kigoma wakiwa katika kikao, Picha na Emmanuel Seny

Mkuu wa Mkoa Kigoma Thobias Andengenye ameyataka mashirika yasiyo ya Serikali kufanya kai kwa kuzingatia sera na miongozo ya katiba ya nchi katika kuwahudumia ikiwa ni pamoja na kuweka wazi shughuli wanazozifanya.

Na Josephine Kiravu

Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza majukumu kupitia miradi mbalimbali mkoani Kigoma yametakiwa kujikita maeneo ya vijijini na kutoa huduma zenye kubeba vipaumbele vya wananchi.

Akifungua Mkutano wa mashirika hayo  kimkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameutaka uongozi wa mashirika hayo kushirikisha walengwa kabla ya kuamdaa na kutekeleza mipangokazo yao.

Amesema pamoja na mchango mkubwa wa mashirika hayo uliofikia Shilingi bilioni 24 kwa mwaka 2023, kwa ajili ya kuwezesha miradi ya kutolea huduma kwa jamii, bado baadhi yameshimdwa kuwasilisha taarifa za utendaji kazi wao kwa mamlaka zinazosimamia uratibu wa kazi zao hali inayotilia shaka utendaji kazi wao.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akizungumza na viongozi wa mashirika yasiyo ya serikali, Picha na Emmanuel Senny

Kupitia hotuba yake, Andengenye amewataka viongozi wa Mashirika hayo kuzingatia miongozo na sheria za nchi ili kudumisha uwazi na uwajibikaji katika Jamii.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, Mwantumu Mahiza amesema kumekuwepo na mashirika hewa yanayojitambulisha kufanya kazi zake mkoani Kigoma huku mengine kazi zake zikiwa hazina tija kwa jamii zaidi ya kunufaisha watendaji badala ya wananchi.

Amesema baadhi ya mashirika hutumia fursa za kuwapiga picha wakazi masikini na mazingira yao kisha kuchukua picha hizo kwenda kuombea fedha kwa wahisani na kujinufaisha wenyewe na kuwa hili halikubaliki hata kidogo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, Mwantumu Mahiza, Picha na Emmanuel Senny

“Kupitia kikao hiki kila kiongozi wa Shirika atapata nafasi ya kueleza kazi wanazotekeleza, changamoto na mafanikio. Hii itatusaidia kutambua ukweli na kuimarisha dhamira ya kuliinua taifa letu” amesema  Mahiza.