Joy FM

‘Wananchi bado wana uelewa mdogo wa kisheria’

24 January 2025, 08:42

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa na baadhi ya viongozi baada ya kuzugnumzia kampeni ya msaada wa kiseheria

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wananchi kujitokeza kushiriki kwenye kampeni ya Mama Samia Legal Aid ili waweze kupata elimu ya masuala ya kisheria.

Na Josephine Kiravu

Imeelezwa kuwa uelewa wa kisheria kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya kijijini bado ni mdogo hali ambayo ianatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wananchi kukosa haki zao ikiwemo masuala ya mirathi.

Hayo yameelezwa na Dawati la msaada wa kisheria kutoka halmashauri ya wilaya ya Buhigwe pamoja na wakili Prosper Maghaibuni ambao wamesema bado hali si shwari kwa upande wa uelewa wa wananchi kuhusu sheria na kwamba baadhi ya migogoro imekuwa ikifikishwa mahakamani licha ya uwezekano wa kumaliza migogoro hiyo ngazi ya chini.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye akizungumza na wanahabari amesema kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aids wananchi mkoani Kigoma watapata msaada wa kisheria kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ukatili pamoja na mirathi na kupunguza migogoro ya ardhi.

Awali akizungumza na wataalamu mbalimbali wakiwemo mawakili, maafisa dawati na wengine ambao watakwenda kutoa elimu kwa wananchi Mkurugenzi wa kitengo cha huduma za kisheria Wizara ya katiba na sheria Ester Msambazi amesema wanatarajia kuifikia mikoa 11 nchini ikiwemo Kigoma Geita na Kilimanjaro na matarajio yao ni kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza hususani wanawake, watoto na makundi maalumu mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.

Kampeni ya utoaji wa msaada ya kisheria ya mama Samia Legal Aid inafanyika kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia mwezi march 2023 hadi mwezi feb 2026 katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar