Serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu
6 December 2024, 12:18
Pichani ni waziri mkuu wa Tanzania Kassimu Majaliwa akiwa kwenye mahafali ya 43 ya chuo kikuu Huria cha Tanzania ambayo yamefanyika Mkoani Kigoma
Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kasimu Majaliwa amesema serikali itaendelea kuunga mkono kwa vitendo sekta ya Elimu hasa elimu ya juu inayotolewa nchini ili kuweza kuwa na wataalamu wabobevu wa kada mbalimbali watakaosaidia nchi kuleta mapinduzi ya viwanda yatakayosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi.
Na,Lucas Hoha
Ni katika mahafali ya 43 ya chuo kikuu Huria cha Tanzania ambayo yamefanyika Mkoani Kigoma ambapo jumla ya wahitimu elfu 4,307 wamemaliza masomo kutoka kanda mbalimbali ikiwemo wabobevu wa masuala ya Diplomasia ya kimataifa na wanataaluma wa masuala ya sheria
Mgeni rasmi katika mahafali hayo Kassimu Majaliwa ametumia nafasi hiyo kueleza masuala mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu na miongoni mwa masuala hayo amesema kuna kila sababu ya wanazuoni kuwa wabunifu na kutengeneza mitaala itakayosaidia kuzalisha wasomi wenye ujuzi nakulisaidia Taifa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo huria cha Tanzania Profesa Elifasi Tozo Bisanda amesema chuo hicho kitaendelea kutoa elimu bora na kuzalisha wataalamu wenye uwezo wakushindana kwenye soko la ajira na kuleta mageuzi ya viwanda nchini na nchi jirani.
Naye Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Professa Kaloline Nombo amesema wizara hiyo itaendelea kubuni sera za uboreshaji wa Elimu nchini, huku Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la zimamoto na Uokoaji Thobisa Andenege ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza mkoani kigoma kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali za uwekezaji.