Wananchi wataka serikali kuharakisha ujenzi wa daraja mto Ruiche Kigoma
18 November 2024, 12:40
Serikali kupitia kwa wakala wa barabara za mijiji na vijijini TARURA Wilaya Kigoma imesema inaendelea na ujenzi wa daraja la mto ruiche ambalo limekuwa likiwasumbua wananchi wa eneo hilo hasa wakati wakivuka kwenda shuleni.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Wananchi wa Kata ya Kagera hasa wanaoutumia mto Ruiche kuvuka kwenda maeneo ya Mgumile wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa daraja ili kurahisiah kufika eneo la mgumile kwa urahisi na kuondoa hofu kutokana na usafiri wa mtumbwi wanaotumia kwa sasa kutokuwa rafiki.
Febraury 24, 2023 ni siku ambayo ina kumbukumbu mbaya kwa wakazi wa kitongoji cha mgumile kata ya Kagera baada ya watoto 6 kuzama mto ruiche wakati wakivuka kuelekea shuleni na mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvuka kupigwa na dhoruba na kupinduka.
Hali hiyo iliamsha hisia za wananchi na kuiomba Serikali kuwajengea daraja, na aliekuwa mkuu wa wilaya kwa wakati huo Salum Kali kuahidi kujenga daraja kwenye eneo hilo.
Na sasa ujenzi unaendelea lakini wananchi ni kama bado hawaelewi hatma yao kwani hulazimika kuahirisha shughuli zao mto ukiwa umejaa maji.
Kwa upande wake, Meneja wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Mhandisi Paul Mtapima amesema ujenzi unaendelea na matarajio ni kukamilika February 2025.
Hata hivyo kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo unatajwa kurejesha matumaini kwa wanafunzi ambao wengi wao walilazimika kuhamishwa shule huku ikiwa ni ahueni pia kwa wazazi pamoja na wananchi wa maeneno hayo kwani shughuli kubwa wanayoitegemea ni kilimo katika eneo la mgumile.