Serikali yaomba wananchi kushiriki miradi ya maendeleo
13 November 2024, 13:55
Mkuu wa wilaya ya Kigoma Dkt Rashid Mohamed Chuachua akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa shule Gungu
Mkuu wa wilaya ya Kigoma Dkt Rashid Mohamed Chuachua amewataka wananchi kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kupunguza gharama za miradi hiyo.
Na, Esperancer Ramadhan
Dkt. Chuachua ameyasema wakati akizindua ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Gungu iliyopo manispaa ya Kigoma Ujiji na kusema kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu kwani ni chanzo cha kuchochea maendeleo ya miradi hiyo.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mkuu wa shule ya msingi Gungu Bw. Octavian Rutasha amesema kuwa wanufaika wakubwa wa mradi huo ni wanafunzi wapatao 180 hali ambayo itapunguza mrundikano wa wanafunzi darasani.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kata ya Gungu wameishukuru serikali kwa kuanza ujenzi wa madarasa hayo kwani uchache wa madarasa ulikuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo ulianza tarehe 8 mwezi 11 mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 8 mwezi 2 mwaka 2025 ambapo madarasa 4 na matundu 6 ya choo yatajengwa kupitia mradi huo.