Wahitimu FDC Kasulu watakiwa kuwa wabunifu kujipatia kipato
28 October 2024, 13:03
Katibu tawala wilaya Kasulu Mkoani Kigoma Bi. Theresia Mtewele amesema tayari serikali imefungua zoezi la utoaji wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halamshauri kupitia mapato ya ndani na hivyo vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi hawana budi kuchangamkia fulsa hiyo ili kujipatia kipato kupitia mikopo hiyo.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wahitimu wa mafunzo ya ufundi kwa kozi fupi na kozi ndefu katika chuo cha maendeleo ya wananchi Kasulu FDC mkoani Kigoma wametakiwa kubuni vyanzo mbalimbali vitakavyowasaidia kujiingizia kipato ili kunufaika na Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Katibu tawala wilaya ya Kasulu Bi Theresia Mtewele Akiwa mgeni Rasmi katika mahafali ya 39 ya chuo hicho amewataka vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi kuchangamkia Fursa za mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.
Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi kasulu FDC Bi.Fridegarda Mukyanuzi amesema jumla ya wasichana 200 wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ufundi kupitia mradi wa Wezesha binti unaofadhiriwa na Shirika la Enabel kutoka Serikali ya Ubeligiji.
Aidha mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho,Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye amewataka vijana hao kutumia ujuzi wao kuleta matokeo chanya Katika Familia.
Kwa upande wao baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali wameeleza namna watakavyo buni na kuchangamkia fursa mbalimbali za kujiingizia kipato.
Jumla ya wanachuo 310 wanatarajia kuhitimu kozi fupi na kozi ndefu kwa fani mbalimbali ambapo kati ya hao wanachuo wa kozi fupi 184 maarufu wanagenzi katika program ya kukuza ujuzi nchini inayowezeshwa na Serikali ya Tanzania na kuratibiwa na Ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana na watu wenye ulemavu huku wanachuo 26 wakiwa wamefadhiliwa na Shirika la world vision Tanzania.