Watendaji watakiwa kuwa wabunifu utoaji wa chakula shuleni
24 October 2024, 09:06
Serikali wilayani Buhigwe imesema inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kusimamia suala la chakula shuleni ili wanafunzi waweze kupata chakula.
Na Emmanuel Kamangu – Buhigwe
Mwenyekiti wa kamati ya lishe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina ameagiza watendaji wa kata zilizofanya vibaya kwenye utoaji wa chakula shuleni kuongeza ubunifu ili kutimiza lengo la Serikali chini ya Mh. Dkt. Samia Suruhu Hasani la kumaliza tatizo la lishe nchini.
Kanal Ngayalina amesema hayo wakati akipokea taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na tathimini ya viashiria vya mkataba wa lishe kwa wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Bw. George Mbilinyi amesema watendaji wa kata wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa mfano katika kukabiliana na tatizo la lishe bora kwa wanafunzi na familia zao kwa ujumla.
Naye Afisa lishe wilaya ya Buhigwe Bi. Melina Jombe amesema kwa kiasi kikubwa chakula kinachotolewa shuleni kimesaidia kuendelea kuimarisha hali ya lishe bora kwa wanafunzi na kuhimiza kata zote wilayani humo kusimamia vyema ulaji wa chakula shuleni.
Aidha Bi. Jombe ameongeza kuwa kitengo cha lishe wilayani Buhigwe kitaendelea kusimamia kikamilifu swala la lishe bora kuanzia ngazi ya familia ili kukabiliana na udumavu kwa watoto.