Wananchi wafurahia huduma za madaktari bingwa Kasulu
9 October 2024, 13:04
Madaktari bingwa ambao wanaendelea kutembea kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa sehemu ya mpango wa serikali wa kuhakikisha wanaboresha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi nchini.
Lucas Hoha – Kasulu
Wananchi wa Halmashuri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wamepongeza hatua ya serikali kuwaruhusu madaktari bingwa wa Dkt Samia Suluhu Hassan kutembea mikoani na kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutoa matibabu kwani itasaidia wananchi kupata matibabu ya kibingwa karibu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wagonjwa waliojitokeza kupata matibabu ya kibingwa kwenye hospitali ya Mji wa Kasulu Mlimani, wamesema awali walikuwa wanashindwa kusafiri kwenda kufuata huduma za kibingwa kutokana na kipato kidogo, huku wakiomba serikali kuangalia namna ya kubeba matibabu hayo kwa zaidi ya asilimia 70 kwani kaya nyingi hapa nchini bado ni masikini.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali ya mji wa Kasulu Jafari Nawabu amesema madaktari bingwa hao watatoa matibu kwa muda wa siku 6 kwa lengo la kuhakikisha wananchi wenye changamoto za magonjwa wanapata matibabu ya uhakika nakuwa mji wa kasulu una wagonjwa wengi wanaohitaji matibabu ya kibingwa.
Kwa upande wake kiongozi wa madaktari bingwa hao ambao wamefanya kambi katika mji wa kasulu Dkt Innocent Kaiza amesema kwa muda wa siku hizo wanauhakika watafikia malengo, huku akiwaomba wananchi wa mji wa kasulu na maeneo jirani kujitokeza kupata matibabu hayo ili taifa liwe na watu wenye afya watakaosaidia kuleta maendeleo.
Madaktari bingwa hao kutembea kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhakikisha wanaboresha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi kwa kuwafikia wananchi wenye changamoto ya magonjwa mbalimbali na miongoni ya matibabu ya kibingwa yatakayotolewa katika kambi hiyo ni magonjwa ya wanawake, upasuaji, matibabu ya mifupa na magonjwa ya ndani