Wazazi watakiwa kuwezesha watoto kupata elimu bora
4 October 2024, 13:27
Serikali imewataka wazazi na walezi kuendelea kuwapeleka watoto wao shule ili kupata elimu itakayowasaidia kuweza kutimiza ndoto zao.
Na Lucas Hoha – Kasulu DC
Wazazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwalea watoto wao katika maadili mema na kutimiza wajibu wao kwa kuwawezesha watoto kupata elimu bora ili waweze kufikia ndoto zao nakuwa raia wema kwenye jamii watakaosaidia kuchochea maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Banki ya NMB Wilaya ya Kasulu Ipyana Mwakatobe ambaye ni mgeni rasmi kwenye mahafari ya 11 ya wahitimu katika shule ya sekondari Magaba iliyopo kata ya Nyakitonto Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Mwakatobe amesema wapo baadhi ya wazazi wanaosahau wajibu wao kwa watoto nakupelekea baadhi ya watoto kushindwa kufikia ndoto zao na wengine wanajikuta wanatumia dawa za kulevya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Magaba Leonard Reubeni Magaba amesema lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo nikuwasaidia wafunzi kupata elimu bora na kuwasaidia watoto wanaoshi kwenye mazingira magumu ili waweze kupata elimu kupitia shule hiyo.
Akisoma Risala kwa niaba ya Wanafunzi Modesta Phanuel amesema kwa muda wa miaka minne wamejifunza vitu mbalimbali ikiwemo kupinga ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto, kutunza mazingira na kufanya kazi kwa bidii, huku wakitoa ahadi kwa wazazi kuwa watakuwa raia wema watakaosaidia kuleta maendeleo.
Shule ya sekondari Magaba iliyopo kata ya Nyakitonto Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ilianzishwa mwaka 2011 na katika mahafari hayo ya 11 jumla ya wanafunzi 45 wanatarajia kufanya mtihani wa taifa.