Wananchi watakiwa kujiandikisha kupiga kura Kibondo
30 September 2024, 13:04
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya kibondo mkoani kigoma amewataka wananchi wilayani humo kuhakikisha wanajitokeza na kujiandikisha ili waweze kushiriki kwenye zoezi la upigaji kura.
Na James Jovin – Kibondo
Wananchi wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha ili kuweza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika kote nchini mwishoni mwa mwezi November ili kuweza kuwachagua viongozi bora na hivyo kujiletea maendeleo
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa halimashauri ya wilaya ya Kibondo bw. Deoclets Rutema wakati wa mkutano wa kuhamasisha upigaji kura na kutoa elimu uliofanyika katika Kijiji cha Kigina kata ya Rugongwe.
Aidha amesema kuwa ili kuwapata viongozi bora katika serikali za mitaa ni lazima wananchi wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi lakini pia kuchagua hali ambayo itawaletea maendeleo katika maeneo yao kwa kuongozwa na viongozi sahihi.
Awali afisa uchaguzi katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo bw. Daniel Ndarangavye amewataka wananchi kutambua kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ni tofauti na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani hivyo vitambulisho vya mpiga kura havitatumika badala yake wapiga kura wataandikishwa katika vitongoji vyao.
Aidha wananchi wametakiwa kutambua kuwa ili kumpata kiongozi bora wanapaswa kujiweka kando na mgombea anayetoa rushwa lakini pia mpiga kura pamoja na wagombea wa nafasi zote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania.