Mbunge agawa majiko 200 ya gesi kwa wajasiriamali Kibondo
26 September 2024, 09:54
Serikali imesema itaendelea kuhamasisha wananchi kujua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha utunzaji wa mazingira nchini unaendelea kwa kugawa mitungi ya gesi katika makundi mbalimbali ya wajasiriamali na mama ntilie na baba ntilie.
Na James Jovin – Kibondo
Mbunge wa Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma amegawa majiko ya gasi yapatayo 200 kwa wajasiriamali, mama ntilie na baba ntilie katika kata zote 19 zinazounda jimbo hilo kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali za kutunza mazingira na kupunguza ukataji wa mito ovyo.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa majiko hayo mbunge wa Jimbo la Muhambwe Dr. Florence Samizi amesema kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha ifikapo 2033 asilimia 80 ya watanzania wote wawe wanatumia nishati safi na salama ya kupikia.
Aidha amesema kuwa yeye kama mbunge wa jimbo la Muhambwe hana budi kuunga mkono jitihada za rais Samia Suluhu Hassan katika malengo ya serikali ya kutunza mazingira na kuhakikisha jamii inaishi mahali salama lakini pia vizazi vjavyo kwa ujumla.
Kwa upande wao baadhi ya wajasiliamali na mama lishe waliopokea msaada huo wa majiko ya gasi wameshukuru kwa msaada huo na kwamba itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira katika mazingira yao.
Katika hatua nyingine mbunge wa jimbo la Muhambwe DR. Florence Samizi amesema kuwa nishati ya kuni imekuwa ikisababisha kwa kiasi kikubwa madhara kwa binadamu na viumbe mbali mbali hivyo mpango wa kusaidia wananchi kutumia majiko ya gass ni mkombozi kwa jamii ya watanzania.