Mabalozi EU wahimiza wakimbizi Nyarugusu kupata haki zao
26 September 2024, 08:35
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya umoja wa mataifa wameendelea kuhamasisha wakimbizi waliopo kwenye kambi za Nyarugusu na Nduta mkoani Kigoma ili waweze kurejea kwa hiari katika nchi yao ya asili ambayo ni Burundi.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Mabalozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika nchi za Burundi na Tanzania wamezindua mradi wa Cross Border katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma kwa lengo la kuhakikisha wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kwa hiari wanapata huduma stahiki kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
Balozi wa EU nchini Tanzania Christine Grau amesema wataendelea kuzisaidia kambi za wakimbizi nchini Tanzania na kuhakikisha wakimbizi wanaorejea nyumbani wanapata haki za msingi kama raia wengine ambapo amesisitiza kuwa euro milioni 40 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 121 za Kitanzania zimetolewa katika kuhakikisha wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao wanapata mahitaji yao muhimu.
Balozi wa umoja huo nchini Burundi Elizabetta Pietrobon amezishauri nchi za Tanzania na Burundi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha wakimbizi wa Burundi wanarejea nchini mwao kwa hiari kwa ajili ya kulijenga taifa hilo ambapo ameendelea kuwatoa hofu kuwa kwasasa taifa hilo kuna amani.
Aidha Mkurugenzi wa Urejeaji wa Wakimbizi nchini Burundi Bw. Nestory Bimenyimana amesema katika taifa hilo wameshaweka mazingira rafiki kwa wakimbizi wanaorejea nchini mwao kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi nchini Tanzania Sudi Mwakibasi ameeleza kuwa amani iliyopo nchini Burundi ni ya kutosha hivyo wakimbizi wa Burundi wanatakiwa kujiandikisha kurejea nchini mwao.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameendelea kusisitiza wakimbizi wa Burundi kurejea nyumbani kwa kuwa changamoto ya usalama iliyokuwepo kwa sasa haipo tena katika taifa hilo.