Wakristo watakiwa kuliombea Taifa
17 September 2024, 11:30
Wakristo Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kuliombea Taifa ili Mungu aweze kuliepusha na matatizo yanayoendelea kujitokeza ikiwemo mauwaji na utekaji wa watu Nchini.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mkoani Kigoma Mhasham Emmanuel Bwatta amewataka waumini wa dini ya Kikristo mkoani Kigoma kuiombea nchi ya Tanzania kuendelea kuwa na amani na upendo ili Mungu aweze kuiepusha na matukio mbalimbali yanayoendelea hapa nchi ikiwemo suala la utekaji na mauwaji.
Askofu Bwatta ameyasema hayo katika ibada ya uzinduzi wa kanda mpya ya Kaskazini yenye makao makuu yake kata ya Nyachenda halmashauri ya wilaya Kasulu.
Amedai zipo kauli zinazozungumzwa ambazo zimekuwa zikitofautia kutoka kwa baadhi ya wanasisasa, watumishi wa Mungu na viongozi wa serikali kuhusu suala vitendo vya uhalifu vinavyoendelea hapa nchini na kuwataka waumini hao kuiachia serikali ndiyo iweze kutolea majibu huku wakiendelea kuliombea taifa kuendelea kuwa na amani.
Aidha Askofu Bwatta amesema anaimani serikali inafuatilia kujua chanzo cha matatizo hayo ili iweze kuyatatua huku akiwasihi waumini hao kuachana na mihemko ya kisiasa na kiimani.
Kwa upande mkurugenzi wa kanisa la Anglikana kanda ya Shunga mchungaji Canon Shedrack Ntabebela amesema yote yanawezekana pale unapomuomba Mungu kwa bidii pasipo kuingia kwenye migogoro yoyote.
Nao baadhi ya waumini wa dini ya Kikristo mkoani Kigoma wamesema ili taifa liweze kuwa na amani umoja pamoja na hofu ya Mungu vinahitajika katika jamii.