Joy FM

Mvua yaziacha kaya 25 bila makazi Kigoma

6 April 2026, 12:33

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua akiangalia nyumba iliyoanguka baada ya mvua kubwa kunyesha, Picha na Hamis Ntelekwa

Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia April 5, 2026 ikiambatana na upepo imesababisha nyumba kuanguka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuacha wananchi bila makazi.

Na Mwandishi wetu

Zaidi ya kaya 25 katika kata za Majengo na Kipampa Manispaa ya Kigoma Ujiji, zimepoteza makazi baada ya nyumba zao kubomoka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana Aprili 5, 2026 na kuharibu miundombinu ya kutiririsha maji na kusababisha maji kusambaa kwenye makazi ya watu.

Kufuatia hali hyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa aliyefika katika maeneo yaliyoathirika, ametoa maagizo kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuchukua hatua za dharura ili kukabili hali hiyo ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kutokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Sauti ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, ametembelea na kuwafariji wananchi waliothiriwa na mafuriko hayo na kueleza hatua za awali zilizochukuliwa huku akiwasihi wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kutathimini madhara yaliyotokea ili kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kurekebisha miundombinu iliyoharibika.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua akiangalia nyumba iliyoanguka baada ya mvua kubwa kunyesha, Picha na Hamis Ntelekwa

Baadhi ya wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo, wameeleza namna mvua ilivyoleta athari katika makazi yao huku wakiomba msaada kwa serikali.

Kwa upande, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Musa Maulid, amethibitisha kuwa madhara yaliyotokea yamesababishwa na kutokamilika kwa ujenzi wa mfereji unaotoa maji katika bwawa la Katubuka kuelekea ziwani.

Sauti ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Musa Maulid,
Mkuu wa Wilaya Kigoma akiwa na wananchi wakati wakizunguka kuangalia nyumba zilizoanguka kutokana na mvua, Picha na Hamis Ntelekwa