Joy FM
Joy FM
3 April 2026, 15:52

Wenyeviti wa mitaa pamoja na mabalozi wametakiwa kuongeza juhudi katika kudhibiti vitendo vya ukatili vinavyoendelea kujitokeza katika jamii. Hayo yameelezwa kufuatia ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia, majumbani na dhidi ya watoto katika baadhi ya maeneo.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, amewataka wenyeviti wa mitaa kufanya kazi na mabalozi na makundi mengine ndani ya jamii ili kuweka mikakati ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti ambavyo vinazidi kukithiri wilayani humo.
Mheshimiwa Dkt. Chuachua, amesema hayo katika kikao na wenyeviti, watendaji wa mitaa, madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, pamoja na watendaji wa idara nyingine za serikali, kilicholenga kutathimini kazi iliyofanyika kwenye kliniki ya ardhi ya kusikilza na kutatua kero a ardhi katika wilaya ya Kigoma.
Amewaagiza viongozi kufanya mikutano na wananchi ili kutoa elimu na kukemea vitendo vya ukatili.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, amewataka wenyeviti wote wa serikali za mitaa kuwabaini wanunuzi wa ardhi katika maeneo yao ili kuhakikisha wanaonunua ardhi ni raia wa Tanzania tu.
Amesisitiza kuwa watu ambao siyo raia wa Tanzania hawaruhusiwi kumiliki ardhi na kwamba ni muhimu viongozi kuwaelimisha wananchi kuwa ardhi ni mali ya watanzania.