Joy FM
Joy FM
30 March 2026, 09:13

Usafi wa mazingira ni jambo muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu, mazingira yanajumuisha sehemu tunazoishi, tunazofanyia kazi, pamoja na maeneo ya kijamii kama vile shule, masoko na hospitali.
Na Mwandishi wetu
Mkuu Wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, amezielekeza mamlaka zinazosimamia usafi wa mazingira katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wasiotekeleza jukumu la kufanya usafi katika maeneo ya makazi yao au biashara zao.
Dkt. Chuachua amesema ametoa maelekezo hayo mwishoni mwa juma, wakati alipowaongoza wafanyabashara katika soko la Masanga kufanya usafi ndani ya soko hilo, kama sehemu ya kuwakumbusha wafanyabiashara hao na wananchi wote kwa ujumla wajibu na umuhimu wa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao.
Amesema suala la usafi wa mazingira ni la lazima hususan katika maeneo ya huduma za kijamii, akisisitiza kuwa atakayebainika kupuuzia suala hilo atakumbana na adhabu stahiki.
Nike Masoud, Katibu wa Wauza Dagaa katika soko la Masanga, na Joram Kinyuko, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Soko la Masanga, wameshauri serikali kuboresha miundombinu ya soko hilo kama hatua mojawapo ya kudumisha usafi wa mazingira ndani ya soko hilo.