Joy FM
Joy FM
27 March 2026, 13:08

Ujenzi wa masoko ni njia muhimu ya kuwawezesha wafanyabiashara kukua na kuboresha maisha yao pamoja na maendeleo ya jamii nzima.
Na Hagai Ruyagila
Wananchi wa Mtaa wa Kanazi, Kata ya Ruhita Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wameiomba serikali kuwajengea banda la soko ili kuwawezesha kufanyia biashara zao katika mazingira salama zaidi.
Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo, ambapo wameeleza kuwa wanakumbana na changamoto kubwa wakati wa msimu wa mvua na jua kali.
Wamesema hali hiyo imekuwa ikiathiri shughuli zao za kibiashara na kupunguza kipato chao, wameeleza kuwa kukosekana kwa banda la soko kunawalazimu kufanya biashara zao katika mazingira yasiyo rafiki, hali inayosababisha usumbufu mkubwa hasa nyakati za mvua zinaponyesha au jua kali linapozidi.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Ruhita, Juma Hindanya, amesema suala la ujenzi wa banda la soko tayari limeshawasilishwa kwenye bajeti ya serikali, na hatua za utekelezaji zinaendelea kufanyiwa kazi endapo bajeti ikiruhusu.

Naye, Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Ruhita Leonard Yohana amekiri uwepo wa changamoto hiyo kwa wafanyabiashara wa soko la Kanazi. Huku akibainisha namna ambavyo serikali imejipanga kutatua changamoto hiyo, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Wodi ya wazazi katika zahanati ya Kanazi.
