Joy FM
Joy FM
26 March 2026, 13:17

Shirika la Catholic Relief Services (SRC) limeendelea kuwakutanisha makundi mbalimbali ya wananchi kwa lengo la kuwapa elimu ya uchumi rejeshi ili kusaidia kutunza mazingira na kuhifadhi maji ya ziwa Tanganyika
Na Mwandishi wetu
Wakazi wa Mkoa wa Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika taka wanazozalisha kwa kuzigeuza kuwa chanzo cha kipato kupitia dhana ya uchumi rejeshi, hatua itakayosaidia kuboresha mazingira pamoja na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Pauline Ndigeza, wakati wa mkutano wa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaojihusisha na uchumi rejeshi uliofanyika Mkoani Kigoma.

Ndigeza amesema kuwa taka ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikionekana kama kero, zinaweza kuwa rasilimali muhimu iwapo zitatumika ipasavyo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kubadili mtazamo wao.
“Ni wakati sasa kwa wakazi wa Kigoma kuona taka kama fursa ya kiuchumi badala ya mzigo hii itasaidia kuongeza kipato na kulinda mazingira yetu,” amesema Ndigeza.
Kwa upande wao, baadhi ya wajasiriamali wanaojishughulisha na uchumi rejeshi wameeleza kuwa tayari wanatumia fursa hiyo kujipatia kipato, ingawa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji ya kuendeleza shughuli zao.

Mmoja wa wajasiriamali hao amesema kuwa pamoja na jitihada wanazofanya katika ukusanyaji na uchakataji wa taka, bado wanahitaji msaada wa kifedha ili kupanua biashara zao.
“Tunafanya kazi ya ukusanyaji na uuzaji wa taka zinazoweza kurejelezwa, lakini changamoto kubwa ni mikopo ya kuendeleza shughuli zetu,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa shirika la misaada la Catholic Relief Services (CRS) Kigoma Joseph Siminzile amesema kuwa tayari kuna fursa za mikopo kwa wajasiriamali hao, huku dirisha la maombi likiwa limefunguliwa.

Amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao na kuongeza mchango wao katika utunzaji wa mazingira.
“Kuna fursa za mikopo kwa wajasiriamali wa uchumi rejeshi na dirisha lipo wazi. Tunawahimiza kujitokeza kwa wingi kuomba ili waweze kuimarisha shughuli zao,” amesema mtaalamu huyo.

Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika mkoa wa Kigoma pamoja na kulinda rasilimali muhimu ikiwemo Ziwa Tanganyika, ambalo lina mchango mkubwa kwa maisha ya wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Mradi wa VOICES ni mradi wa miaka minne ukitekelezwa katika nchi za Tanzania na Zambia katika eneo la Mpumalanga ukiwa na lengo la kutunza mazingira na maji ya ziwa Tanganyika kwa kuzigeuza taka kuwa fursa kupitia uchumi rejeshi.