Joy FM

Bilioni 2.6 zajenga kituo cha afya Makere Kasulu

24 March 2026, 12:05

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa na baadhi ya viongozi wengine wakati akikagua mradi wa kituo cha afya Makere, Picha na Mwandishi wetu

Serikali kupitia Wizara ya afya imeendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa wananchi

Na Mwandishi wetu

Jumla ya shilingi bilioni 2.6 zimetumika kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Makere katika kijiji cha Makere Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Kukamilika kwa kituo hicho kutaondoa changamoto kwa wananchi wa kata hiyo kutegemea huduma za matibabu kutoka kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo Wilayani humo.

Muonekano wa kituo cha afya Makere, Picha na Mwandishi wetu

Meneja wa Wakala wa barabara Mkoa Kigoma, Mhandisi Chora Kimata amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya miradi 12 ya nyongeza inayotokana na mradi mkubwa wa barabara ya kiwango cha lami ya Manyovu Wilaya ya Buhigwe hadi Kabingo Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma.

Mhandisi Kimata amesema kuwa mradi huo ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/S Ottonde Construction & General Supplies kwa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umefikia asilimia 97 ya utekelezaji wake na tayari mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 1.7.

Akizungumzia kutekelezwa kwa mradi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Samuel Kadogo amesema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Makere ambao awali msaada mkubwa wa matibabu ilikuwa kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambako ilibidi kuingia kwa vibali.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mipango ya serikali kusogeza huduma kwa wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.