Joy FM

Kituo cha zana za kilimo chazinduliwa kusaidia wakulima Uvinza

13 March 2026, 14:01

Mkuu wa Wilaya Dinnah Mathaman akiwa katika uzinduzi wa zana za kilimo Nyanganga Uvinza, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Zana za kilimo ni vifaa vinavyotumika kurahisisha shughuli za kilimo kama kulima, kupanda, kupalilia na kuvuna na zina umuhimu mkubwa kwa wananchi hasa wanaotegemea kilimo kama chanzo cha maisha.

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Kijiji cha Nyanganga, Kata ya Kazuramimba, Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma wameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwainua wakulima kupitia uzinduzi wa Kituo cha Zana za Kilimo kitakachosaidia kupunguza utegemezi wa jembe la mkono.

Akizungumza katika kikao na wananchi wa kijiji hicho, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amesema Serikali imeanzisha kituo hicho kwa lengo la kurahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima ili waweze kulima maeneo makubwa zaidi na kuongeza uzalishaji.

Mkuu wa Wilaya Uvinza akiendesha moja wapo ya zana za kilimo zilizozinduliwa kijiji cha Nyanganga Uvinza, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Mh. Dinah ameeleza kuwa tayari Serikali imeleta power tiller (pawatila) ambayo itatumika kuwasaidia wakulima katika shughuli za maandalizi ya mashamba kuelekea msimu wa kilimo, hatua itakayochochea kilimo cha kisasa na chenye tija kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Uvinza, Ndg. James Mkumbo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo vizuri kwa kulima kilimo chenye tija kitakachosaidia kuinua uchumi wa familia na jamii kwa ujumla.

Miongoni mwa zana zilizozinduliwa, Pcha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Naye Diwani wa Kata ya Kazuramimba, Mh. Mussa Chessa, kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo ameishukuru Serikali kwa kuthamini juhudi za wakulima wa eneo hilo na kuanzisha kituo hicho, akieleza kuwa kitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wananchi.

Mh. Musa amesema wananchi wa kata hiyo wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kituo hicho kinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wakulima na maendeleo ya jamii.