Joy FM
Joy FM
12 March 2026, 17:00

Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha maendeleo ya Mkoa wa Kigoma yanafikia azma ya serikali ya dira ya maendeleo ya 2050
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, amesema Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuhakikisha Taifa linafikia maono na matarajio yaliyomo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipofungua kikao kilichoikutanisha Serikali ya Mkoa na wadau wa maendeleo kutoka Sekta binafsi, kilicholenga kujadili hatua mbalimbali za kukuza uwekezaji, biashara na ukuaji jumuishi wa Uchumi, kilichofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani hapa.

Amesema mabadiliko ya haraka yanapaswa kufanyika kwenye Sekta za biashara na uwekezaji, Kilimo, Mifugo, Uvuvi na shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ujasiriamali ili kutoa fursa kwa wananchi kuzidi kunufaika kiuchumi.
“Kuboresha Mazingira ya ujasiriamali ni njia pekee ya kukabiliana na changamoto ya ajira na kuwaondoa wananchi katika utegemezi wa ajira rasmi kwa ajili ya kuendesha maisha yao” amesisitiza Sirro.
Amesema wataalam kutoka Sekta za Umma na zile binafsi wanapaswa kuwasaidia wananchi katika kuondoa vikwazo dhidi ya fursa za kiuchumi huku akisisitiza mkoa kuwa na mazingira rafiki kibiashara kutokana na kuendelea kuimarika kwa miundombinu wezeshi kiuchumi ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, upatikanaji wa uhakika wa Umeme sambamba na kuanzishwa kwa Ukanda Maalum wa Uchumi Kigoma (KiSEZ).

Upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Enabel nchini, Koenraad Goekint amesema mageuzi endelevu ya kiuchumi, yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi binasi huku akisisitiza kuwa, mabadiliko ya kiuchumi yanapaswa kuwanufaisha wananchi wote huku nguvu kubwa ikielekezwa zaidi kwa wanawake na vijana.
Kikao hicho kilichoenda sambamba na mjadala wa pamoja wa wadau hao, kimeandaliwa na Shirika la Maendeleo la watu wa Ubelgiji (Enabel) chini ya Mradi wa wezesha binti, kimewakutanisha zaidi ya wadau 30 wa Maendeleo kutoka Sekta ya biashara, Taasisi za Umma na binafsi, Taasisi za Fedha na wajasiriamali wanawake.
