Joy FM
Joy FM
10 March 2026, 14:43

Biashara haramu ya binadamu ni moja ya matatizo makubwa ya kijamii yanayoikumba dunia ya leo kwa kusafirisha, kudanganya au kulazimisha watu kufanya kazi au vitendo fulani kwa manufaa ya watu wengine bila ridhaa yao.
Na Mwandishi wetu
Wazazi na walezi Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana kikamilifu katika malezi ya watoto ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu hususani watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Akizungumza na Radio Joy, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya Kasulu Inspekta Maimuna Omary amesema ushirikiano wa wazazi na walezi ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama na kuepukana na vitendo vya ukatili pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu.
Ameeleza kuwa baadhi ya watoto husafirishwa kwa kisingizio cha kupelekwa kufanya kazi au kusomeshwa hali ambayo wakati mwingine inahatarisha usalama, haki na ustawi wa watoto hao.
Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kasulu wamesema bado uelewa wao ni mdogo katika kutambua viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kutolewa elimu kwa jamii ili kulinda watoto na kukomesha vitendo hivyo.