Joy FM
Joy FM
9 March 2026, 08:12

Ukatili ni tatizo kubwa katika jamii nyingi na unaweza kutokea majumbani, shuleni, kazini au katika maeneo ya umma, mara nyingi wahanga wa ukatili hukosa msaada kwa sababu watu wanaoshuhudia au wanaojua kuhusu vitendo hivyo hushindwa kutoa taarifa.
Na Mwandishi wetu
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vya ukatili vinavyotendeka dhidi ya wanawake na watoto ili kudumisha ulinzi na usalama kwa makundi hayo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani ambapo kimkoa yamefanyika wilayani Kakonko.

Amesema kutoa taarifa kwa wakati dhidi ya matukio hayo, kutasaidia kuepusha kupoteza ushahidi na haki kwa wanaodhulumiwa kupatikana kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Mathamani amewataka wanawake kuongeza ubunifu katika kuibua mawazo ya miradi ya maendeleo kabla ya kuomba mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri ili biashara wanazoanzisha ziweze kustawi na kuwaletea tija.

Amesema ili kuibua mawazo ya biashara au kutekeleza shughuli nyinginezo za ujasiriamali kwa ufanisi, wanapaswa kushirikiana na wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwa karibu zaidi sambamba na kubaini iwapo shughuli za kiuchumi wanazoanzisha zipo katika mazingira sahihi.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa barabara zinazouunganisha mkoa na mikoa jirani pamoja na uwepo wa umeme wa uhakika, kumeongeza kwa kiasi kikubwa fursa za kimasoko ndani ya mkoa na kulitaka kundi hilo kuzitumia fursa hizo.
