Joy FM
Joy FM
5 March 2026, 12:03

Uadilifu ni mojawapo ya sifa muhimu kwa viongozi wa umma hasa watendaji wa vijiji na kata ambao ni viongozi wa karibu zaidi na wananchi katika ngazi za serikali za mitaa.
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amewataka watendaji wa kata kusimamia kwa uadilifu na uwajibikaji mchakato wa ajira zinazotokana na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotarajiwa kupita katika wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao kazi cha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kilichohusisha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na watumishi wa utawala, Kanali Mwakisu amesema ajira hizo zinalenga kuwanufaisha wakazi wa kata na wilaya zitakazopitiwa na reli, huku fomu maalumu zikitarajiwa kutumika kuthibitisha waombaji wa kazi hizo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu Theresia Mtewele, amesisitiza umuhimu wa watendaji kusoma mapato na matumizi katika maeneo yao ili kupanga mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Awali, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Alpa Eliatosha, amewaasa washiriki kuepuka tabia zisizofaa kama kamari na ulevi wa kupindukia akisema ni muhimu kuzingatia maadili ya kazi.
Takribani watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira mbalimbali, zikiwemo nafasi za nguvu kazi, kazi za kawaida, na nafasi maalumu kwa akina mama kuongoza magari na watembea kwa miguu wakati wa utekelezaji wa mradi huo