Joy FM
Joy FM
2 March 2026, 12:09

Elimu ni msingi muhimu katika maendeleo ya mtoto na taifa kwa ujumla hata hivyo katika mchakato wa kujifunza, kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa masomo darasani ikiwemo ni tatizo la watoto kukaa chini kwa kukosa madawati.
Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Mkoani Kigoma Prof. Pius Yanda kupitia mfuko wa Jimbo hilo amechangia shilingi milioni 2 kutatua changamoto ya uhaba wa madawati Katika shule ya msingi Nyamingunga iliyopo kata ya Muyama ili kumaliza tatizo la watoto kusoma wakiwa wamekaa chini.
Hayo yamejiri wakati wa Ziara ya Mbunge wa jimbo la Buhigwe Prof. Pius Yanda katika kata ya Muyama kwa lengo la kuwashukuru na kuzungumza na wananchi ambapo mmoja wawananchi Maria Kiloloma ameomba kutatuliwa kwa changamoto ya Watoto kukaa chini katika shule hiyo na kueleza kuwa wazazi wanachangia kiasi cha shilingi elfu 3 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya utengenezaji wa madawati ya Shule hiyo.

Akitolea ufafanuzi wa wazazi kuchangia shilingi elfu 3, Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Nyamingunga Mwl. Baraka Ahmed amesema zoezi hilo limefanyika kutokana na uwepo wa baadhi ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini kwasababu ya upungufu wa madawati hivyo wakakubaliana kwa kila mzazi kuchangia kiasi hicho ili kutatua changamoto ya madawati katika shule hiyo.

Kufuatia uwepo wa changamoto hiyo, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Prof.Pius Yanda amesema atachangia shilingi milioni 2 ili kuunga mkono juhudi za wazazi katika kukabiliana na Uhaba wa madawati Katika shule hiyo.