Joy FM
Joy FM
27 February 2026, 12:42

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka Kanda ya magharibi ili kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya BoT, udhibiti wa mikopo umiza, na umuhimu wa kutumia taasisi ndogo za kifedha zilizosajiliwa
Na Josephine Kiravu
Benki kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Magharibi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuelewa na kutafsiri kwa usahihi majukumu na kazi za benki hiyo katika uchumi wa taifa.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yameanza Mkoani Kigoma yamehusisha mikoa ya
Kigoma, Katavi, Kagera na Tabora lengo likiwa ni kuwawezesha wanahabari hao kuchambua na kuandaa habari kuhusu masuala ya fedha na uchumi kwa ufasaha.
Awali akifungua mafunzo hayo, Meneja msaidizi wa Uhusiano wa umma, Benki kuu ya Tanzania (BoT) Bi. Noves Moses amewataka wanahabari hao kutumia vyema mafunzo hayo na kwenda kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.

Kupitia mafunzo hayo mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa ikiwemo namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo nchini, muundo na majukumu ya Benki hiyo ambapo imeelezwa kuwa jukumu lake la msingi ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha nchini kwa lengo a kudhibiti mfumko holela wa bei na kuhakikisha utulivu wa uchumi nchini unakuwepo.
Aisha amesema wanatarajia kuona jamii ikipata uelewa juu ya huduma ndogo ndogo za fedha na utambuzi wa alama kwenye noti.
Hata hivyo kupitia mafunzo hayo BoT inatarajia kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu sera na shughuli zake kupitia taarifa sahihi na zenye uchambuzi makini