Joy FM

Dawati la jinsia kudhibiti utumikishwaji watoto kwenye biashara

23 February 2026, 12:37

Baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara, Picha na Mwandishi wetu

Watoto ni hazina ya taifa na msingi wa maendeleo ya baadaye ya jamii yoyote hivyo wanahitaji malezi bora, elimu, ulinzi na mazingira salama ili waweze kukua kimwili, kiakili na kimaadili licha ya kuwa bado kuna changamoto ya watoto kutumikishwa kwenye shughuli za biashara wakiwa chini ya umri unaoruhusiwa kisheria.

Na Michael Mpunije

Jeshi la Polisi dawati la Jinsia na Watoto Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaondoa Watoto wanaofanya shughuli za biashara chini ya umri wa miaka 18 ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya Watoto.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Murusi, Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kasulu Inspekta Maimuna Omary amesema zoezi hilo litakuwa endelevu ili kuhakikisha Watoto wanaofanya shughuli hizo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo wanachukuliwa hatua za Kisheria.

Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya Kasulu Inspekta Maimuna Omary, Picha na Mwandishi wetu

Amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika suala la Malezi kwa kutimiza wajibu wao kwa Watoto ikiwa ni Pamoja na kuwaandikisha shuleni Watoto wote wenye umri wa kuanza masomo.

Sauti ya Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya Kasulu Inspekta Maimuna Omary

Afisa ustawi wa jamii Halmashauri ya mji Kasulu, Tausi Baraka ameitaka jamii kushirikiana kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na Ukatili kwa kwa Watoto kwa kutoa taarifa za vitendo hivyo kwenye mamlaka husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaobainika.

Afisa ustawi wa jamii Halmashauri ya mji Kasulu, Tausi Baraka, Picha na Mwandishi wetu