Joy FM

RAS Kigoma ataka wataalamu wa afya kufanya kazi kwa weledi

13 February 2026, 16:18

Katibu tawala Mkoa Kigoma akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa idara ya afya kutoka halmashauri za Kigoma, Picha na Sadick Kibwana

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amewataka wataalamu wa afya Mkoani Kigoma kufanya kazi kwa weledi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali

Na Sadick Kibwana

Zaidi ya wajawazito 3,000 wanatarajia kunufaika na kitita jumuishi cha afya ya uzazi salama kwa Mama na Mtoto  Mkoani Kigoma mpango ambao unatajwa kuboresha huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Wajawazito hao ni kutoka katika Wilaya za Kigoma, Kibondo, Kakonko, Kasulu, Buhigwa na Uvinza watanufaika kupitia mradi huo wa kitita cha afya ya mama na mtoto mkoa wa kigoma.

Baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa katika kikao kazi cha afya katika Ukumbi wa Joy In The Harvest, Picha na Sadick Kibwana

Akizungumza katika Ufunguzi wa Mradi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa, amewataka wataalamu wa kada ya afya kuendelea kutimiza malengo ya mradi kwa mshikamano.

Aidha Rugwa amesema kila kitu kuhusu mradi huo kimekamilika kilichobaki ni wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya ya Mama na Mtoto Wizara ya Afya Dk Felix Bundala, amesema kumekuwa na changamoto ya uzazi hivyo kuzinduliwa kwa mradi huo utasaidia kupunguza kwa sababu umeshaonesha mafanikio sehemu mbalimbali.

Kitita cha uzazi salama ni jumuisho la mbinu kadhaa kuboresha afya kwa kupunguza vifo vya mama na watoto wakati na baada ya kujifungua pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa kutumia vifaa tiba na vifaa vya mafunzo vilivyoboreshwa.

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza wakati wa kikao na wadau wa afya, Picha na Sadick Kibwana