Joy FM
Joy FM
27 January 2026, 08:04

Wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kijitokeza na kuwasaidia vijana wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kufikia ndoto zao
Na Mwandishi wetu
Shirika la Maendeleo la watu wa Ubelgiji (Enabel) kupitia Programu ya wezesha binti, limekabidhi vifaa mbalimbali vyenye Thamani ya Shilingi Mil. 794 kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu na washindi kitaalum katika halmshauri tano za mkoa wa Kigoma.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Matenti 13, baiskeli 270, vifaa vya michezo pamoja na madaftari kwa wanufaika hao katika halmashauri za Kigoma Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya mji na Wilaya Kasulu pamoja na Kibondo.
Mara baada ya kupokea vifaa hivyo kutoka kwa mfadhili huyo na kuvikabidhi kwa Wakuu wa Wilaya katika maeneo lengwa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro anasema mradi wa wezesha binti umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza elimu jumuishi kwa kuwagusa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Amesema vifaa hivyo vitapunguza utoro na kuimarisha mazingira ya kujifunza na kujifunzia hususani kwa watoto wa kike na kuongeza fursa ya kuzifikia ndoto zao za kielimu.

Vifaa hivyo ikiwemo matenti yametolewa kwa ajili ya kuwapatia faragha watoto wa kike katika mazingira ya shuleni, baiskeli kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wanafunzi wanaoishi makazi yaliyo mbali na shule, pamoja na vifaa vya michezo vyenye lengo la kuimarisha afya, ushirikiano na kujiamini.