Joy FM
Joy FM
26 January 2026, 15:50

Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kata ya Itebula Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma wameomba serikali na wadau kuwasaidia baada ya nyumba zao kuezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo na kusababisha nyumba na mali zao kuharibika.
Na Timotheo Leonard
Mvua kubwa iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali katika Kijiji cha Itebula Kata ya itebula Halmashauri ya wilaya ya uvinza Mkoani Kigoma, imesababisha madhara kwa wananchi wa eneo hilo ambapo nyumba zaidi ya ishirini zimeezuliwa na upepo na kuwaacha bila makazi ya kuishi.

Protas Guzuye ambaye ni Mtendaji wa Kiijiji cha itebula kata ya Itebula akizungumza na Radio Joy fm kwa njia ya simu, amesema chanzo cha kuezuliwa kwa nyumba hizo ni mvua iliyoambatana na upepo mkali na kusisitiza wananchi kupanda miti ili kupunguza madhara.
Kwa upande wake , Batromeo Sigaya mwenyekiti wa Kitongoji cha Chemchem kata ya Nguruka yeye anasimlia namna mvua ilivyoanza kunyesha kwa karibu saa moja na kwamba wananchi hawanabudi kuzingatia ubora wakati wa ujenzi wa nyumba zao.

Baadhi ya wakazi wa kata ya itebula Tarafa ya Nguruka Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza wameiomba serikali kuendelea kushikamana na wananchi waliopata madhara kutokana na mvua hiyo.

Aidha mamlala ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA inaendelea kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za mvua pamoja na kufuatilia utabiri wa hali ya hewa wakati wote ilikuepuka madhara yanayoweza kuepukika.
