Joy FM
Joy FM
16 January 2026, 15:35

Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma Mwalimu Paulina Ndigeza amewataka walimu kuhakikisha wanafundisha matumizi ya msingi wa awali (baseline) ili kuwajengea uwezo wanafunzi wa somo la kingereza
Na Hagai Ruyagila
Walimu wakuu pamoja na walimu wa kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo maalum ya matumizi ya baseline kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa wa somo la Kiingereza kabla ya kuanza masomo mengine ya kidato cha kwanza.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma, Mwalimu Paulina Ndigeza, katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Bogwe iliyopo mjini Kasulu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwl. Ndigeza amesema kuwa ni wajibu wa kila mwalimu wa kidato cha kwanza kuanza na somo la baseline ili kumsaidia mwanafunzi kupata uelewa wa lugha ya Kiingereza, ambayo ni lugha ya kufundishia katika ngazi ya sekondari.
Amesema hatua hiyo itamwezesha mwanafunzi kumudu masomo mengine pindi anapoanza masomo rasmi ya kidato cha kwanza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Upendo Lugumila, amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu.
Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuboresha uelewa wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wengi ambao wamekuwa na changamoto ya lugha hiyo, huku masomo mengi yakifundishwa kwa Kiingereza.
Baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini, unaolenga kumjengea mwanafunzi msingi imara wa lugha ya Kiingereza ili aweze kujifunza kwa ufanisi masomo ya sekondari.
