Joy FM
Joy FM
8 January 2026, 14:23

Serikali wilayani Kakonko mkoani Kigoma kupitia TANTRADE imesema itawasaidia wakulima wa zao la mhogo kutafuta masoko ili waweze kuuza zao ndani na nje ya nchi na kuwa na soko la uhakika.
Na Josephine Kiravu
Wafanyabiashara wa zao la mhogo wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamesema baada ya uzalishaji wa zao hilo kuwa juu imepelekea kukosa wanunuzi wa zao hilo jambo ambalo limewaibua TANTRADE na kulazimika kufanya nao kikao na kutembelea ghala za kuhifadhia zao hilo ili kuona namna ya kuwasaidia wazalishaji wa zao hilo.
Taarifa zaidi na Josephine Kiravu
Wakizungumza wakati wa kikao hicho baadhi ya wafanyabiashara wamesema kwa sasa wameyumba kiuchumi kutokana na kukosa soko kwa ajili ya zao hilo.
Kwa upande wake Petrol Matulanya ambae ni Afisa biashara mwandamizi TANTRADE ameahidi kuwatafutia masoko zaidi ndani na nje ya nchi kwani uzalishaji umeongezeka na wanunuzi ni wale wale.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Viwanda na Biashara mkoani Kigoma Deogratius Sangu amesema kupitia TANTRADE wazalishaji na wafanyabiashara wa zao la mhogo wataanza kunufaika na kuondokana na changamoto zinazowakabili kwa sasa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amewataka wakulima kuendelea kuzalisha kwa wingi zao hilo huku akiwatoa hofu kuhusu upatikanaji wa soko kwani tayari TANTRADE wameahidi kutafuta wanunuzi wa zao hilo.