Joy FM
Joy FM
8 January 2026, 13:08

Ujenzi wa vibanda vya biashara kwa ajili ya wajasiriamali vinavyoendelea kujengwa kando ya barabara vimetajwa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wamekuwa wakipata changamoto ya mvua na jua wakati wa biashara zao.
Na Lucas Hoha
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro ameagiza viongozi wanaosimamia ujenzi wa vibanda vya kufanyia biashara kwa ajili ya akina mama wajasiriamali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kukamilisha ujenzi huo na ifikapo Januari 10, 2026 vianze kutumika.
Sirro ametoa maagizo hayo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua vibanda hivyo na kuona hatua iliyofikiwa ili kuwanusuru akina mama hao kufanya kazi kwenye mazingira magumu kwani mvua na jua vimekuwa sehemu ya maisha yao.
Amesema vibanda hivyo vimejengwa kwa ufadhili wa shirika la maendeleo ya Ubelgiji nchini Tanzania Enabel mara baada ya uongozi wa mkoa kuwaomba kuwasaidia kujenga vibanda hivyo.
Akizungumzia kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa vibanda hivyo na ujenzi wa miundombinu mengine ikiwemo upatikanaji wa maji, uwepo wa choo na Umeme Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkoa Fransisco Magoti amesema tayari wamesharatibu masuala mhimu ya kulipa maji, ujenzi wa choo na kulipia umeme.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kasulu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu CPA France Kafuku amepongeza jitihada zilizochukuliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa za kujenga vibanda hivyo kwani ni hatua mhimu inayoonyesha serikali kuwajali wananchi.