Joy FM
Joy FM
17 December 2025, 07:59

Mamlaka ya usimamizi wa chakula na vifaa tiba Tanzania TMDA Kanda ya Magharibi imesema itaendelea kufanya operesheni mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti bidhaa za afya zinazoingizwa nchi kinyuma cha sheria na ambazo hazikidhi vigezo
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Chakula na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Kanda ya Magharibi, kuongeza kasi katika kusimamia ubora na udhititi bidhaa za kiafya ili kulinda afya za wakazi kutokana na mkoa kupakana na nchi jirani, jambo linaloweza kutoa mianya kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza bidhaa tiba mkoani hapa bila kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Balozi Sirro amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa TMDA, ofisini kwake leo Desemba 16, 2025 na kusisitiza kuwa, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu unatakiwa kuzidi kufanyika ili kubaini dawa feki na bidhaa za kiafya qzisizo na viwango zinazoingizwa nchini kinyume na sheria kabla ya kuleta athari kwa watumiaji wa mwisho.

Ameipongeza mamlaka hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya katika kuendelea kusimamia uzalishaji wa bidhaa za kiafya na chakula kwani utimamu wa Afya za wananchi ni kichocheo kikubwa cha Maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Meneja wa TMDA Kanda ya Magharibi Christopha Osward amesema, mamlaka hiyo inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa, vituo vya Afya, Hospitali pamoja na kutoa Elimu kwa wadau wa Afya kuhusu utambuzi na matumizi sahihi ya vifaa tiba na dawa.

Amesema mamlaka itaendelea kushirikiana na wataalam wa Afya ngazi ya mkoa na mamlaka za Serikali za mitaa katika kuhakikisha wanatoa huduma bora na yenye kukidhi viwango vya utoaji wa huduma kwa jamii.