Joy FM
Joy FM
13 December 2025, 12:03

Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha inaimarisha utunzaji wa vyanzo vya maji
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema jamii inapaswa kuendelea kutunza vyanzo vya Maji ili serikali iweze kufanikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo Kichwani kupitia utekelezaji wa Miradi mikubwa ya Maji.

Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua mradi wa Maji Munanila-Nyakimue unaotekelezwa na Serikali wilayani Buhigwe mkoani hapa huku akiupongeza uongozi wa Wilaya hiyo kwa kuimarisha na kutekeleza kwa vitendo Sheria ya Mazingira inayohusu uhifadhi wa vyanzo vya Maji.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa maji mkoani Kigoma unafikia Asilimia Mia Moja ambapo hadi sasa hali ya upatikanaji wa huduma hiyo kimkoa ni Asilimia 86, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la upatikanaji wa huduma hiyo katika wilaya ya Buhigwe na Mkoa kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Buhigwe Golden Katoto amesema, mradi unatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu kiasi cha Shilingi bilioni 9.7 na shilingi bilioni 5 ikiwa ni fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ikiwa ni utekelezaji miradi ya nyongeza kutokana na ujenzi wa barabara ya Kasulu hadi Manyovu kwa kiwango cha lami.
Amesema mpaka kufikia Desemba 12, 2025, mradi umekamilika kwa asilimia 83 na umeanza kutoa huduma katika vijiji vya Bweranka na Kibande, ambapo jumla ya kaya 261 zimeunganishwa na huduma ya maji majumbani sambamba na upatikanaji wa maji katika mabomba ya mitaani.
