Joy FM

Kigoma Dc yatwaa tuzo ya uwasilishaji bora hesabu za fedha 2024

5 December 2025, 22:56

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akipokea tuzo ya mshindi wa pili ilikwenda kwa Halshauri ya Wilaya Kigoma, Picha Ofisi ya mawasiliano Wilaya Kigoma

Nidhamu ya kitaaluma na utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika kuimarisha mifumo ya fedha na uwazi wa taarifa vimetajwa kuchochea Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutunukiwa tuzo ya mshindi wa pili ya uwasilishaji bora wa fedha kwa mwaka 2024

Na Mwandishi wetu

‎Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imepata heshima kubwa baada ya kutunukiwa Tuzo ya Mshindi wa Pili (2nd Winner) katika Kundi la Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia shindano la Best Presented Financial Statements Award kwa mwaka wa fedha 2024, lililoandaliwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

‎Tuzo hiyo imetolewa tarehe 4 Desemba 2025 ikiwa ni sehemu ya kutambua Halmashauri zilizofanya vizuri zaidi katika uandaaji, uwasilishaji na uzingatiaji wa viwango vya kitaifa vya usimamizi wa fedha za umma katika hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam.

‎Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Balozi Simon Sirro na Viongozi wengine ngazi ya Mkoa walipata fursa ya kuungana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba aliyeambatana na Mweka Hazina wa Halmashauri CPA Enock Shilinde katika kukabidhiwa tuzo hiyo.

‎Kupatikana kwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa utendaji bora, uwajibikaji na uadilifu wa timu ya wataalam wa fedha pamoja na uongozi mzima wa Halmashauri katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi na kwa kufuata taratibu.

‎Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imeeleza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya kazi ya pamoja, nidhamu ya kitaaluma na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuimarisha mifumo ya fedha na uwazi wa taarifa.

‎Kigoma DC inaendelea kujipambanua kama miongoni mwa Halmashauri zinazofanya vizuri nchini katika usimamizi wa fedha za umma hatua inayotoa hamasa ya kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akipokea tuzo ya mshindi wa pili ilitwaliwa na Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Picha na Ofisi ya mawasiliano wilaya Kigoma