Joy FM
Joy FM
5 December 2025, 14:28

Serikali imewataka watendaji wa Serikali za mitaa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya maendeleo
Na Hagai Ruyagila
Maafisa Watendaji wa serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya maendeleo ya taifa na kuepuka kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye mitaa wanayoisimamia
Wito huo umetolewa na Kaimu mkuu wa Wilaya ya Kasulu Bw. Ibrahimu Mwangarume wakati akizungumza na baadhi ya maafisa watendaji wa serikali za mitaa wa halmashauri hiyo.
Amesema ni wajibu wa watumishi wa umma kuwa mabalozi wa wazuri wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuchochea maadili mema katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye amewataka watendaji hao kuendeleza uadilifu katika kazi zao ili kujijengea heshima na kuaminika zaidi mbele ya wananchi wanaowaongoza.
Naye mwenyekiti wa watendaji wa serikali za mitaa katika halmashauri ya Mji Kasulu Bw. Leonard Lugunguja amesema wataitumia mitandao ya kijamii kama fursa ya kujiongezea kipato na siyo kama chanzo migogoro au vurugu katika jamii.
