Joy FM

World vision yakabidhi madarasa mapya na vyoo Kasulu

26 November 2025, 15:47

Mkuu wa Wilaya Kasulu akiwa na wanafunzi katika picha na wakati World vision ikikabidhi madarasa, Picha tovuti ya Kasulu

Shirika la World Vision Tanzania limekabidhi madarasa na vyoo kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu ikiwa nisehemu ya kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya elimu

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaack Mwakisu, amelipongeza Shirika la World Vision kwa mchango wake katika kuboresha mazingira ya elimu baada ya kukamilisha ujenzi wa madarasa manne na matundu 10 ya vyoo katika shule za msingi Tulieni na Chashenze.

Akizungumza leo, Jumatano Novemba 26, 2025, katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shule ya Msingi Tulieni, Kata ya Makere, Kanali Mwakisu amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 238.8 ni hatua muhimu katika kuinua ustawi wa jamii na kuleta mabadiliko chanya kwa watoto wa eneo hilo.

Jengo la matundu ya vyoo yaliyokabidhiwa na World Vision kwa Halmashuri ya Kasulu, Picha na tovuti ya Kasulu

“Niwashukuru sana World Vision. Miundombinu kama hii mnayotujengea si tu inawawezesha watoto wetu kusoma katika mazingira bora na salama, bali pia inaongeza matumaini ya kutimiza ndoto zao. Mmeisaidia sana serikali ambayo ina majukumu mengi katika maeneo tofauti ya nchi,” amesema Mwakisu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, amesema mradi huo umeunga  juhudi za serikali kwa vitendo katika kusogeza maendeleo kwa wananchi kwa kuhakikisha elimu inatolewa kwenye mazingira yenye hadhi na ubora unaotakiwa.

Muonekano wa darasa lililokabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Picha na tovuti ya Kasulu

Meneja Miradi wa Shirika la World Vision Wilaya ya Kasulu, Ester Mushendwa, amesema miundombinu hiyo itawanufaisha wanafunzi 764 wavulana 375 na wasichana 389 pamoja na walimu ambao sasa watatumia ofisi zenye mazingira mazuri na rafiki kwa kazi za ufundishaji.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tulieni, Ibu Ugasa, ameeleza kuwa madarasa hayo mapya yatapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wanafunzi darasani na kuboresha mahudhurio, hasa kutokana na kuwekwa kwa madirisha ya vioo ambayo yanasaidia kuwalinda watoto dhidi ya baridi.

Mkuu w Wilaya Kasulu akizungumza mara baada ya kukabidhiwa madarasa na World Vision, Picha na tovuti ya Kasulu

_