Joy FM

Wanamabadiliko wa kupinga ukatili wapewa baiskeli 100 Kasulu

25 November 2025, 17:08

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye akikabidhi baiskelikwa wanamabadiliko, Picha na Hagai Ruyagila

Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili kwenye jamii, wanamabadiliko wa masuala ya ukatili wa kijinsia wamepewa baiskeli ili waweze kuwafikia wahanga wa vitendo hivyo.

Na Hagai Ruyagila

Shirika la Kivulini kwa kushirikiana na shirika la Plan International chini ya ufadhili wa shirika la Enabel, limekabidhi jumla ya baiskeli 100 kwa wanamabadiliko 100 wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Halmashauri ya Kasulu Vijijini na Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma.

Katika hafla ya ugawaji wa baiskeli hizo, wanamabadiliko kutoka kata tano za Kasulu Mjini na kata tano za Kasulu Vijijini wamekabidhiwa baiskeli 50 kwa kila halmashauri. Lengo kuu ni kuwawezesha kufikisha elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na kuhamasisha hatua za kukabiliana na vitendo hivyo.

Meneja wa Mradi wa Wezesha Binti kutoka Shirika la Kivulini, Bi. Grace Mussa, amesema utoaji wa baiskeli hizo unalenga kuongeza ufanisi wa wanamabadiliko katika kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ili kusaidia kupunguza matukio ya ukatili katika mkoa wa Kigoma.

Sauti ya Meneja wa Mradi wa Wazesha Binti kutoka Shirika la Kivulini, Bi. Grace Mussa
Meneja wa Mradi wa Wazesha Binti kutoka Shirika la Kivulini, Bi. Grace Mussa, Picha na Hagai Ruyagila

Mgeni rasmi katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, amewataka wanufaika baiskeli hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu madhara ya ukatili ili kuchochea maendeleo na ustawi bora wa Taifa.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kumsenga Kasulu Mjini, Rozina Mengo, na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kurugongo Kasulu Vijijini, Essau Henyula, wamesema baiskeli hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa kuwezesha wanamabadiliko kuwafikia wanajamii wengi zaidi na kutoa elimu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Sauti za watendaji

Akizungumza kwa niaba ya wanamabadiliko wenzake, Bi. Elizabeth Mbodo kutoka Kata ya Kumsenga, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha malezi ya watoto na jamii kuendelea kuzingatia maadili mema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl Vumilia Simbeye katika picha ya pamoja na wanamabadiliko, Picha na Hagai Ruyagila

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wanamabadiliko wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kutoa elimu kwa jamii.

Sauti za wanamabadiliko