Joy FM
Joy FM
22 November 2025, 09:31

Wahitimu wa fani mbalimbali katika chuo cha uhasibu ndaki ya Kigoma wametakiwa kuendelea kuwa wabunifu ili waweze kujiajiri na kuacha kuendelea kusubiri kuajiriwa na serikali au mashirika binafsi.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wahitimu wa kozi mbalimbali katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Kigoma, kutumia elimu waliyopata kuisaidia jamii mkoani hapa katika kufanya ubunifu na kusambaza ujuzi wa usimamizi wa biashara ili shughuli za kiuchumi zinazofanyika ziwe na tija kubwa.
Sirro amesema hayo wakati wa mahafali ya 23 ya TIA Kampasi ya Kigoma yaliyofanyika katika majengo mapya ya Kampasi hiyo yaliyo eneo la Kamara Kata ya Mngonya Halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma, ambapo jumla ya wahitimu 756 wametunukiwa cheti cha awali na Diploma katika kozi mbalimbali za uhasibu, usimamizi wa rasilimali watu, ugavi na manunuzi.

Mkuu huyo wa Mkoa Kigoma alisema kuwa kuwa, muhitimu haina maana ya kupata cheti lakini cheti hicho kitakuwa na thamani kama elimu iliyopatikana itatumika kuisaidia jamii hasa watu wa kipato cha chini walio wengi kufanya shughuli zao kwa tija na kuweza kuinua kipato chao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa amesema kuwa elimu ya biashara ni msingi mkubwa wa shughuli za binadamu kwani huwaunganisha wenye kipato kikubwa na kidogo katika kuendesha maisha.

Akitoa taarifa kuhusiana na mahafali hayo, Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo alisema kuwa jumla ya wahitimu 756 wametunukiwa vyeti mbalimbali ambapo kati yao wahitimu wa cheti cha awali 262 ,Astashahada wakiwa 251 na Stashahada wapo 243.