Joy FM

RC Sirro ataka wakurugenzi kugeukia ufundishaji kidijitali

21 November 2025, 08:34

Mkuu wa Mkoa Kigoma akipokea na kukabidhi vifa vya kidijitali kwa ajili ya kufundishia, Picha na Lucas Hoha

Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema kutokana na ukuaji wa teknolojia elimu haina budi kutolewa kwa kuzingatiamatumizi ya teknolojia kwa wanafunzi

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa  Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wakurugenzi wa  halmshauri za mkoa Kigoma kuongeza nguvu katika kukuza na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji kwa ngazi mbalimbali za kitaaluma.

Balozi Sirro alisema hayo akikabidhi kwa Wakurugenzi wa halmashauri tatu za mkoa Kigoma, jumla ya seti 27 za Computer mpakato, Projector na  mfumo wa umeme jua na vifaa vingine vinavyosaidia katika kujifunza na kufundishia, vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo la serikali ya Ubelgiji (ENABEL) ili kuchochea ukuzaji Taaluma kupitia njia ya kidijitali mkoani Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa  Kigoma Balozi Simon Sirro akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa vifaa vya kufundishia, Picha na Lucas Hoha

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, Dunia inapoelekea sasa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasilianao ndiyo yamechukua nafasi hivyo kujikita katika mfumo huo kutachangia kuwapa uwezo mkubwa wahitimu katika kuhimili ushindani kwenye soko la ajira.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa alisema ufundishaji unaojumuisha mifumo vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia umechangia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari za serikali na kuufanya mkoa huo kutoa shule mbili katika shule 10 bora zilizofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne mwaka uliopita.

Kutokana na hilo,  Rugwa alisema mkoa umejipanga kuhakikisha unaongeza matumizi ya vifaa vya kidijitali katika kufundishia na kujifunzia.

Awali Mtaalam wa Dijitali katika Elimu  kutoka Shirika la Maendeleo la Serikali ya Ubelgiji (ENABEL), Lotte Van Praet alisema kuwa shirika hilo limekabidhi seti  27 za Computer mpakato, Projector na mfumo wa umeme jua zenye thamani ya shilingi milioni 81 ambazo zitatumika kwenye shule 12 za sekondari na vituo vitatu vya mafunzo endelevu kwa walimu (TRC) kwenye halmashauri za Kigoma, Kasulu na Kibondo.

Mtaalam wa Dijitali katika Elimu  kutoka Shirika la Maendeleo la Serikali ya Ubelgiji (ENABEL), Lotte Van Praet, Picha na Lucas Hoha