Joy FM

RC Sirro atembelea wakazi waliopisha hifadhi Kasulu

27 October 2025, 14:36

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon akizungumza mara baada ya kutembelea wananchi wa kijiji cha Katoto waliopisha hifadhi ya kitalu, Picha na Ofisi ya mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Serikali imesema itahakikisha inapeleka huduma zote muhimu kwa wananchi waliohama kupisha hifadhi ya kitalu cha uwindaji Makere – Uvinza na kuanza makazi mapya katika kitongoji cha Katoto Wilayani Kasulu

Na Mwandishi wetu

Zaidi ya wakazi 800 wamehamisha makazi yao kutoka eneo walilokuwa wakiishi ndani ya Hifadhi ya  Kitalu cha Uwindaji Makere (FR)-Uvinza Open Area na kuhamia kitongoji kilichorasimishwa na Serikali cha Katoto Mpya kilichopo katika kijiji cha Kagerankanda wilayani Kasulu mkoani hapa.

Akizungumza na wakazi  hao, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewapongeza kwa utayari huo huku akisisitiza kuwa,  Serikali itahakikisha huduma zote muhimu zinawafikia tofauti na walivyokuwa wakiishi katika maeneo ya hifadhi ambayo hayakuwa yamerasimishwa kwa ajili ya makazi.

Muonekano wa hifadhi ya kitalu cha uwindaji, Picha na Ofisi na mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Upande wake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amesema mpaka kufikia Oktoba 26, 2025 jumla ya wakazi 886 wametii agizo la serikali na kuhamia katika eneo hilo ambapo lengo ni kuwawezesha kuwahi kuanza kwa msimu wa kilimo.

Akitolea ufafanuzi kuhusu hali ya ujenzi wa miundombi ya kutolea huduma katika eneo hilo, Kanali Mwakisu amesema tayari ujenzi wa Shule ya msingi umeshaanza huku mwekezaji wa kitalu akiwa katika hatua za upimaji ili kuchimba kisima kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa maji safi.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isack Mwakisu akizungumza na wananchi hao, Picha na Ofisi ya mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Kuhusu huduma za umeme na barabara, Kanali Mwakisu amesema tayari uongozi wa wilaya umewasiliana na mamlaka husika na utekelezaji  upo katika hatua ya tathmini ili kupeleka huduma hizo kitongojini hapo.

Amesema sambamba na wananchi hao kuendelea kuhamia eneo hilo, zoezi linaloendelea kwa sasa ni uandaaji wa njia na vituo maalum kwa ajili ya kuondoa mifugo ndani ya hifadhi na kuifikisha kwenye kitongoji cha Katoto mpya.

Kwa upande wao wakazi hao wameishukuru serikali kwa kuwatengea jumla ya hekta 4,446 kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji,  badala ya kuwatoa hifadhini na kuwaacha wakivamia maeneo mengine ambayo hayakurasimishwa kwa ajili ya kuweka makazi yao jambo ambalo lingechangia kuhatarisha usalama wao na mali zao.

Wananchi waliohama kupisha eneo la hifadhi ya kitalu cha uwindaji, Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma

“Tunaiomba Serikali ifanye tathmini na kutuongezea maeneo kutoka ekari tatu hadi tano kwani wengiwetu tunahitajj kumiliki ardhi ya kutosha kwa ajili ya Kilimo na ufugaji” amesema Mariam Sindela, mkazi kitongojini hapo.