Joy FM

RC Sirro ahimiza wananchi kufanya usafi wa mazingira

25 October 2025, 10:21

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akiwa amewasili kituo cha afumya Gungu kuungana na wananchi kufanya usafi wa mazingiza, Picha na Tryphone Odace

Idara ya afya Mkoa wa Kigoma imesema inaendelea kuweka mikakati ya kuhamasisha wananchi kuzingatia suala la usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya mlipuko

Na Tryphone Odace

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira mara kwa mara katika mazingira yao ili waweze kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
Balozi Sirro amesema hayo wakati alipoungana na wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kufanya usafi katika kituo cha afya Gungu zoezi lililoambatana na uhamasishaji wa wananchi kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 29, 2025.
Amesema kuwa usafi wa mazingira unasaidia kuondoa maradhi na kusaidia watu kupoteza maisha kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.

Aidha Balozi Sirro amewahamasisha na kuwataka wananchi kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa nyemelezi ambayo yamekuwa yakiwasumbua wananchi na kuomba waungane na klabu za jogging ili kuwa na miili imara muda wote.

Naye afisa Mkoa wa Kigoma Nespholi Sungu amesema kuwa sheria inawataka wananchi kuhakikisha wanafanya usafi kwani unasaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakilipuka kwenye jamii.
Sungu amesema kuwa suala la usafi kwa wananchi liende sambamba na ujenzi wa vyoo bora na kunawa mikono kwa ajili ya kuepuka magonjwa ya kuhara.

Baahi ya wananchi na vijana wa jogging wamesema kuwa wataendelea kuhamasisha jamii kufanya usafi na mazoezi huku wakipongeza Serikali kwa namna ambavyo imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kusogeza vituo vya kutolea huduma karibu na wananchi.