Joy FM

Jamii yatakiwa kukemea matukio ya ukatili kwa watoto mitandaoni

23 October 2025, 12:41

Viongozi mbalimbali wakiongozwa na afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunuri, Picha na Ofisa ya Mkoa

Licha ya jitihada mbalimbali za Serikali na wadau kutoa elimu ya masuala ya ukatili bado ukatili kwa njia ya mitandao umeonekana kuwa tatizo kwenye jamii

Na Mwandishi wetu

Makundi yenye jukumu la malezi katika jamii yametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi ya mitandao ya kijamii na vifaa wezeshi  kidijitali ili kudhibiti madhara yatokanayo na mifumo hiyo ya teknolojia ya mawasiliano kwa watoto na vijana.

Akiwasilisha mada katika kikao kilichowakutanisha maafisa kutoka Mahakama, Kamati za Usalama, Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii ngazi za Halmashauri na baadhi ya wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Petro Mbwanji ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, amesema ukatili huo hufanyika kupitia matumizi ya teknolojia kupitia vifaa vya kielektroniki ambavyo ni Simu janja, runinga pamoja na kompyuta.

Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Kigoma Petro Mbwanji akiwasilisha maada, Picha na Ofisi ya mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Amesema baadhi ya watoto wanaotumia vifaa hivyo wamejikuta wakiingia katika ushawishi na kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo, uraibu wa matumizi ya mitandao sambamba na ongezeko la mmomonyoko wa maadili katika jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 hutumia mitandao ya kijamii na baadhi yao hukutana na matukio ya ukatili ikiwemo watu wanaowashawishi kushiriki kutenda vitendo visivyo vya kimaadili.

Washiriki wa mafunzo hao, Picha na Ofisi ya mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Awali akifungua mafunzo hayo, Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunuri amesema, jamii inajukumu kubwa la kutambua uwepo wa madhara katika matumizi ya vifaa hivyo ili kuchukua hatua za makusudi katika kudhibiti hali hiyo kupitia kutoa elimu kwa watoto kuhusu matumizi bora ya nyenzo hizo za kiteknolojia.

Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa sehemu muhimu ya kutafsiri maarifa waliyoyapata kwab kutoa elimu jumuishi katika mazingira yao ya utendaji kazi.

Mafunzo hayo yaliyodhaminiwa na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto duniani (UNICEF), yamelenga kuwakutanisha wadau hao ili kuwajengea uelewa, kujadili na kuja na njia bora zaidi zenye dhamira ya kudhibiti na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto mitandaoni.

Washiriki wa mafunzo wakiendelea kujinza maada mbalimbali, Picha na Ofisi ya mawasiliano Mkoa wa Kigoma