Joy FM
Joy FM
11 October 2025, 16:30

Katika kuadhimisha miaka 53 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Hospitali hiyo inatarajia kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuanzia jumatatu ya Oktoba 13 hadi 17 mwaka huu wa 2025
Na Orida Sayon
Zaidi ya wananchi 3500 kutoka maeneo mbalimbali ya Mko wa Kigoma na meneo jirani wanatarajia kupatiwa huduma za matibabu ya kibingwa ambazo zinatarajiwa kutolewa na madaktari bingwa na bingwa bobezi katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari bingwa na Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni Dkt. Joseph Emmanuel Nangawe amesema huduma hizo za kibingwa zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi na madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 25 kutoka kada mbalimbali za afya na kada zaidi ya 15 zitakuwa na wataalamu.

Amesema kambi hiyo inatarajiwa kuanza Oktoba 13 -17 mwa huu wa 2025 katika hospitali ya rufaa ya maweni ikilenga kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wenye shida mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya jirani.
Aidha Dkt. Joseph Emmanuel Nangawe amehimiza wananchi wenye changamoto za kiafya kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata huduma kutoka kwa madaktari bingwa na mabingwa bobezi zilizosogezwa karibu yao ili kuepuka gharama za rufaa ya kwenda mikoa ya nje ya Kigoma ikiwemo Mwanza, Dodoma na Dar es salaam.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na uzazi kwa wanaume Boniface Kilangi ambaye pia ni mratibu wa huduma za kibingwa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni amesema ujio wa madaktari bingwa unatarajia kuzindua pia huduma mpya za uchunguzi wa mfumo wa chakula itakayotoa huduma kwa wenye changamoto ya magonjwa ya ndani ya tumbo.
Kwa upande wake, Dkt. Ashraf Idd Bitalio Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kambi ya kibingwa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni amesema kambi hiyo itaongeza wigo wa utoaji huduma huku huduma hizo zitahusisha wenye bima, wasio na bima na watu wenye kipato cha chini watapata nafasi ya kutibiwa kulingana na utaratibu utakaowekwa.
Ujio wa madaktari bingwa na bingwa bobezi katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni utaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 53 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya maweni ambayo ilianzishwa mnamo mwaka 1972 na imeendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Kigoma na maeneo ya jirani.
