Joy FM
Joy FM
8 October 2025, 12:04

Serikali imeendelea kuwakumbusha wamiliki wa vyombo vya habari kufuata matakwa ya kisheria kwa kuhakikisha wanatumia na kuajiri waandishi wa habari wenye taaluma ya habari.
Na Josephine Kiravu
Wamiliki wa vyombo vya habari mkoani Kigoma wametakiwa kuajiri wanahabari wenye taaluma ya habari, huku wanahabari nao wakitakiwa kutotumika kisiasa sambamba na kuandika habari ambazo haziwezi kuleta chuki kwenye jamii.
Mwana habari wetu Josephine Kiravu na maelezo zaidi
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Kigoma Dr Rashid Chuachua kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa kwenye mkutano wa majadiliano kati ya baraza la habari Tanzania MCT na waandishi wa habari pamoja na viongozi wa Serikali Mkoani Kigoma.
Ameongeza kuwa licha ya uwepo wa Sheria ya Haki ya kupata habari lakini wapo baadhi ya wanahabari ambayo wanafanya kazi zao pasipo kufuata misingi ya kihabari na kwamba kufanya hivyo ni kosa na inaweza kusababisha chuki na machafuko.

Awali akizungumza kuhusu lengo la mkutano huo, Meneja program kutoka Baraza la habari Tanzania (MCT), Josephat Mwanzi amesisitiza uwepo wa ushirikiano baina ya viongozi wanaotoa taarifa na wanahabari kwani wananchi wanatamani kupata taarifa kwa wakati.
“Jamii imekuwa na njaa kubwa ya habari kwa kukosa taarifa sahihi na hii inatokana na uwepo wa taarifa za uzushi na hivyo simameni kuhakikisha mnafikisha taarifa ili jamii na taifa liweze kusonga mbele” amesema Mwanzi.

Nao baadhi ya wanahabari waliohudhuria kwenye mkutano huo wamesema mara kadhaa wamekosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya viongozi lakini kupitia majadiliano ya hii leo itasaidia kupunguza changamoto hiyo.
Hata hivyo kupitia mkutano huo wanahabari wamepatiwa mafunzo kuhusu mada mbali mbali ikiwemo mchango wa vyombo vya habari katika mchakato wa uchaguzi pamoja na Sheria ya Haki ya kupata taarifa.
