Joy FM
Joy FM
2 October 2025, 09:34

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha maisha ya wazee kwa kuwasaidia kupata matibabu na mahitaji mengine muhinu kama sehemu ya kuambua mchango wao katika jamii.
Na Hagai Ruyagila
Baadhi ya wazee katika Halmashauri ya Mji Kasulu wameiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma na kutambua mchango wao muhimu katika jamii hii ni kutokana na kutengwa na jamii pamoja na familia zao.
Hayo yamebainishwa na baadhi ya wazee akiwemo Bi. Agness Bitazi, Bi Tatu Saidi na Bw Iddi Rugiga wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika katika halmashauri ya Mji Kasulu.
Wazee hao wamezungumzia changamoto zinazowakabili kwa kusema kuwa kundi kubwa la wazee linakabiliwa na changamoto za maisha magumu, ukosefu wa huduma za msingi kama vile dawa, malazi na chakula, pamoja na kutopata heshima wanayostahili kutoka kwa familia na jamii kwa ujumla.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Mji Kasulu Dkt. Peter Janga ametolea kwa ufafanuzi wazee wanaotakiwa kuhudumiwa na serikali kwa kupewa dawa na matibabu ya bure.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Sabinus Chaula amesema kuwa serikali kupitia halmashauri hiyo imekuwa ikiendelea kutambua mchango wa wazee na inaweka mikakati ya kuhakikisha wanapata huduma bora kwa kuzingatia mahitaji yao.

Naye, Mkaguzi wa Jeshi la polisi wilaya ya Kasulu Afande Mbaraka Luwongo ametoa wito kwa jamii kuwatambua wazee kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa huku akisisitiza kuwa mchango wao haupaswi kusahaulika.
Maadhimosho ya siku ya wazee duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba Mosi, ikiwa ni fursa ya kutambua na kuheshimu mchango wa wazee katika jamii na taifa kwa ujumla.