Joy FM

Wananchi wachekelea milioni 300 zikijenga wodi ya wazazi Kasulu

19 September 2025, 08:41

Jengo la wodi ya wazazi Kituo cha Afya cha Mwami Ntale, Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za afya ili wananchi waweze kupata huduma karibu na maeneo yao

Na Hagai Ruyagila

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, ameweka jiwe la msingi katika jengo la wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya cha Mwami Ntale, kilichopo Kata ya Heru Juu, Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mwami Ntale, Mgoba John, amesema fedha zilizotolewa zimetumika kujenga wodi ya wazazi pamoja na jengo la kufulia ili kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya karibu na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 300 kutoka Serikali kuu unalenga kutatua changamoto ya kufuata huduma za afya umbali mrefu.

Sauti ya Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mwami Ntale, Mgoba John

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo la wodi ya wazazi kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi amataka uongozi wa kituo hicho kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unakamilika kwa wakati ili huduma zinazolengwa ziweze kutolewa kwa ufanisi.

Sauti ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Heru Juu wamesema kuwa ujenzi wa wodi ya wazazi umepunguza changamoto kwa akina mama wajawazito, ambao sasa wanaweza kujifungua katika mazingira salama.

Sauti ya Baadhi ya wananchi wa Kata ya Heru Juu
Jengo la wodi ya wazazi Kituo cha Afya cha Mwami Ntale, Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 zimebeba kaulimbiu yenye ujumbe thabiti “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”