Joy FM

Ussi akoshwa na mradi wa nyumba za walimu Kasulu

17 September 2025, 15:06

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ally Ussi akizungumza, Picha na Hagai Ruyagila

Katika kuthamini mchango wa watumishi  wa Umma, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kutolea huduma ikiwemo kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya watumishi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao.

Na Hagai Ruyagila

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, ndugu Ismail Ally Ussi, amezindua na kuweka jiwe la msingi katika nyumba moja ya waalimu aina ya 2-in-1 katika Shule ya Sekondari Kasasa, iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma Mradi ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 110.

Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa nyumba hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Tarimo Michael, amefafanua kuwa ujenzi huo umefanyika kwa njia ya “force account” na umekamilika rasmi mwezi Aprili mwaka huu. 

Aidha mhandisi Tarimo ameeleza faida kuuhusu nyumba hiyo kwa waalimu watakaoitumia, akibainisha kuwa itawasaidia walimu kupata makazi bora na hivyo kuimarisha utoaji wa huduma za elimu.

Sauti ya Mhandisi Tarimo Michael
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Tarimo Michael, Picha na Hagai Ruyagila

Kwa upande wake, Kiongozi wa  Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ally Ussi, amepongeza jitihada za serikali katika kuendelea kujenga nyumba za walimu. 

Amesema nyumba hizo ni muhimu sana ili kuhakikisha waalimu wanapata makazi bora, jambo litakalowawezesha kuwahudumia wanafunzi kwa ufanisi na kuleta mafanikio makubwa kitaaluma.

Sauti ya Kiongozi wa  Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ally Ussi

Aidha Ussi amewataka wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Amehimiza wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo na kuboresha maisha katika maeneo yao.

Mwenge wa Uhuru mwaka huu umebeba kaulimbiu yenye ujumbe thabiti “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”