Joy FM
Joy FM
17 September 2025, 09:57

Mwenge wa uhuru umewasili Wilayani Kasulu na unatarajia kupitia na kukagua miradi 14 ya maendeleo
Na Hagai Ruyagila
Jumla ya miradi 14 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.7 inatarajiwa kukaguliwa, kutembelewa na mingine kuwekewa jiwe la msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. Miradi hiyo inajumuisha sekta za elimu, afya, Maji na miundombinu ya barabara.
Akizungumza wakati wa kusoma taarifa ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanal Isaac Mwakisu, amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri mbili za wilaya hiyo ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Kasulu na halmashauri ya Mji Kasulu kwa umbali wa kilomita 123, kuanzia katika viwanja vya Shule ya Msingi Mvugwe hadi katika stand mpya ya Murusi, iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu.
Kanal Mwakisu amesema kuwa anafahamu na kutambua umuhimu wa Mwenge wa Uhuru katika kuhamasisha maendeleo, mshikamano na amani miongoni mwa wananchi, pamoja na kuwa chombo muhimu cha kuhamasisha ushiriki wa jamii katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake katika Wilaya ya Kasulu huku wananchi wakihamasishwa kushiriki kwa wingi katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na mbio hizo.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 ni “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”